Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, ameeleza kuwa ratiba ya mechi za ligi imepangwa kwa kuzingatia taratibu za kikanuni, hasa muda wa mapumziko kati ya mchezo mmoja na mwingine.
Boimanda amesema kimsingi Simba ingeweza kucheza tena Machi 4 au 5 baada ya Dabi ya Kariakoo iliyochezwa Machi 1, kwa kuwa muda wa saa 72 ungekuwa umetimia kama ilivyokuwa kwa baadhi ya timu nyingine.

Hata hivyo, amefafanua kuwa changamoto ilitokana na ratiba ya timu nyingine.
“Coastal Union wao walicheza na Singida Black Stars Machi 2. Hivyo kama wangepangiwa kucheza na Simba Machi 4, maana yake wangekuwa wanacheza chini ya saa 72, jambo ambalo kikanuni si sahihi,” amesema Boimanda.
Ameongeza kuwa hata kama mechi hiyo ingepangwa Machi 5 bado ingekuwa ngumu kwa Simba kwa sababu tayari walikuwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB uliopangwa Machi 7, hivyo muda wa saa 72 usingetimia.
Kwa mujibu wa Boimanda, ratiba zote hupangwa kwa kuzingatia kanuni za ligi pamoja na ratiba za mashindano mengine ili kuhakikisha timu zote zinapata muda unaotakiwa wa kupumzika. ⏱️
Mjadala wa ratiba umeendelea kupamba moto miongoni mwa mashabiki wa soka nchini baada ya Dabi ya Kariakoo kumalizika kwa sare ya 0-0.
