Shirikisho la Soka Duniani FIFA limetangaza mabadiliko mapya ya sheria za mchezo wa soka yatakayoathiri mashindano ya FIFA World Cup, yakilenga kuongeza kasi ya mchezo na kupunguza upotevu wa muda uwanjani.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni sheria ya sekunde 10, ambapo mchezaji anayefanyiwa mabadiliko anatakiwa kuondoka uwanjani ndani ya sekunde 10. Akishindwa kufanya hivyo, mchezaji anayeingia atalazimika kusubiri dakika moja kabla ya kuruhusiwa kuingia.
Pia kuna sheria ya matibabu, ambayo inasema mchezaji atakayeomba matibabu na kusimamisha mchezo atalazimika kutoka nje ya uwanja kwa dakika moja kabla ya kurudi kucheza, isipokuwa katika mazingira maalum.

Aidha, waamuzi watakuwa na uwezo wa kutumia hesabu ya sekunde 5 wakati wa kurudisha mpira uwanjani kwenye throw-in au goal kick. Ikiwa timu haitarejesha mpira kwa wakati, adhabu itatolewa ambapo throw-in itapewa timu pinzani, huku goal kick ikibadilishwa na kuwa kona kwa timu nyingine.
Katika mabadiliko mengine, mfumo wa Video Assistant Referee (VAR) sasa utakuwa na uwezo mpana zaidi wa kupitia maamuzi, ikiwemo kadi ya pili ya njano pamoja na maamuzi ya kona endapo kutakuwa na kosa la wazi.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kuleta uwazi zaidi katika maamuzi ya waamuzi na kuongeza ushindani katika mchezo wa soka.
