Klabu ya Simba SC imetozwa faini ya jumla ya shilingi milioni 15 pamoja na gharama za matengenezo kufuatia msururu wa makosa ya kinidhamu yaliyotokea katika mchezo namba 054 dhidi ya Young Africans SC uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Machi Mosi, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), makosa hayo ni kama ifuatavyo:
• Kuingia Uwanjani kinyume na Taratibu: Simba imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 kwa kosa la kuingia uwanjani kupitia mlango usio rasmi, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
• Kugomea Chumba cha Kuvalia: Klabu hiyo imepigwa faini nyingine ya Sh. 5,000,000 kwa kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia na badala yake kutumia chumba cha mikutano ya wanahabari, kinyume na Kanuni ya 17:20.

• Vurugu za Walinzi: Simba imetozwa faini ya tatu ya Sh. 5,000,000 kufuatia walinzi wake kugombana na kutoleana lugha ya matusi na walinzi wa Young Africans wakati timu hiyo ikiwasili uwanjani, jambo lililochafua taswira ya mchezo. (Klabu ya Young Africans pia imepigwa faini ya kiasi hicho kwa kosa hili).
• Uharibifu wa Miundombinu: Aidha, Simba italazimika kulipa gharama zote za matengenezo ya mlango wa chumba cha mikutano ya wanahabari ambao walinzi wa timu hiyo waliuvunja ili kulazimisha timu kuingia kutumia chumba hicho kuvalia.
Adhabu hizi zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu zinazohusu Taratibu za Mchezo na Udhibiti kwa Klabu (17:62 na 47:1) ili kurejesha nidhamu katika soka la Tanzania.
