Na Clement Shawishi- Geita
Katibu Tawala Msaidizi Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Geita Bw. Charles Chacha amewaasa Maafisa Habari wa Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kuhakikisha wanajiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Chacha ametoa rai hiyo wakati akifunga mafunzo ya uboreshaji wa mfumo wa tovuti za Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwa Mkoa na Halmashauri yaliyofanyika kwa siku tano katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na masuala mengine ya maendeleo ambayo jamii inapaswa kufahamishwa kupitia tovuti za Halmashauri na mitandao mingine ya kijamii kwa weledi.

Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Bw. Best Mgimbwa amesema maboresho ya mfumo wa tovuti yamefanyika ili kuondoa changamoto za kiufundi zilizokuwepo awali kwenye tovuti na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu wanaozisimamia umefanyika ili kuwakuza kitaaluma.
Mgimbwa ameongeza kuwa Tovuti hizo zinalenga kuimarisha utoaji wa taarifa kwa ubora na kwa wakati huku akisisitiza jukumu la Maafisa Habari na TEHAMA kuhakikisha taarifa zote muhimu na matangazo ya Serikali yanawekwa kwenye Tovuti.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Bwn. Frank Mbaga amesema mafunzo hayo yamelenga kuboresha matumizi ya Tovuti za Serikali ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wote Ofisa TEHAMA Halmashauri ya Wilaya ya Geita Charles Mlagaja amepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwa kuona umuhimu wa wataalam wanaoshughulikia Tovuti za Halmashauri kupata mafunzo muhimu kuboresha usimamizi wa Tovuti hizo kulingana na mabadiliko ya teknolojia yaliyopo.

