Baba Mtakatifu Papa Leo XIV, amemteua Konrad Krajewski kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Łódź nchini Poland.
Kabla ya uteuzi huo, Kardinali Krajewski alikuwa Msimamizi wa Sadaka ya Papa na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo.
Kardinali Krajewski alizaliwa tarehe 25 Novemba mwaka 1963 katika mji wa Łódź nchini Poland,Baada ya kujiunga na Seminari ya Jimbo Kuu la Łódź mwaka 1982, alipata shahada ya Taalimungu kutoka John Paul II Catholic University of Lublin na Alipewa daraja la Upadre tarehe 11 Juni mwaka 1988.
Katika utume wake wa kichungaji, Kardinali Krajewski alihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Makamu wa Parokia huko Rusiec na Łódź. Pia alipata mafunzo na leseni ya Liturujia katika Taasisi ya Liturujia ya Kipapa ya Mtakatifu Anselm mjini Roma.
Aidha, aliwahi kuwa mshereheshaji wa Jimbo Kuu la Łódź, na baadaye akawa profesa katika Seminari ya Jimbo pamoja na Seminari za Wafransiskani na Wasalesiani za Jimbo hilo. Pia alifundisha katika University of Warsaw na baadaye akawa Mkuu wa Seminari ya Jimbo Kuu la Warsaw.
Kardinali Krajewski pia ni Daktari wa Taalimungu aliyebobea katika Liturujia kutoka Pontifical University of Saint Thomas Aquinas mjini Roma. Mbali na hilo, aliwahi kuwa msaidizi katika Ofisi ya Maadhimisho ya Liturujia za Kipapa na pia Padre Mhudumu katika kliniki ya mifupa na maumivu ya kiwewe ya Sapienza University of Rome.
Mwaka 2013, aliteuliwa na Pope Francis kuwa Mkuu wa Sadaka ya Baba Mtakatifu na kupokea wakfu wa Kiaskofu tarehe 17 Septemba mwaka huo.
Baadaye, tarehe 28 Juni mwaka 2028, Papa Francisko alimuinua kuwa Kardinali akimkabidhi Kanisa la Maria Asiye na Dhambi la Esquilino.
Tangu mwaka 2022, Kardinali Krajewski alikuwa akihudumu kama Mkuu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo hadi uteuzi wake mpya wa kuongoza Jimbo Kuu la Łódź.
