Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa Ethiopia (CBCE) umelaani vikali wimbi la vurugu dhidi ya raia katika eneo la Arsi, jimbo la Oromia,Katika taarifa iliyotolewa tarehe 9 Machi 2026 na kusainiwa na Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Addis Ababa na Rais wa CBCE, Maaskofu walisema kuwa mashambulizi dhidi ya watu wasio na hatia hayawezi kuhalalishwa kwa misingi ya dini, utamaduni au siasa.
Maaskofu wamesema mauaji na uharibifu unaoendelea ni vitendo visivyo vya kibinadamu na vimesababisha hofu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, Wametoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka ili kuwalinda raia na kurejesha usalama katika maeneo yaliyoathiriwa.
Ripoti zinaonyesha kuwa hali ya usalama imezidi kuwa mbaya katika wilaya za Shirka, Merti, Guna na Holonto katika eneo la Arsi,Wakazi wengi wanaripotiwa kuuawa, kujeruhiwa, kupoteza mali na kulazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yanayoendelea.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, Wakristo 34 wa Kanisa la Kiorthodox waliuawa, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, kutoweka au kutekwa nyara, Mashambulizi hayo yanahusishwa na mgogoro wa mpaka katika jimbo la Oromia ulioanza mwaka 2025 na ambao tayari umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.
Maaskofu pia wametoa wito wa umoja na mshikamano wa kidini, wakihimiza Waethiopia kukataa chuki na mgawanyiko. Wamesisitiza kuwa jamii inapaswa kushirikiana kulinda amani na kuzuia vurugu zinazoendelea kuathiri wananchi.
