
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amewaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha hawawaondoi Waganga Wafawidhi wa vituo vya afya ngazi ya msingi kwa utashi binafsi.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo alipokuwa akihitimisha mkutano wa mwaka wa Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi, uliofanyika Jijini Dodoma kwa siku mbili.
Amewataka Wakurugenzi watumie vigezo vya kupima utendaji au ubora wa kazi za Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya msingi—yaani Key Performance Indicators (KPI)—na si maamuzi ya mtu mmoja mmoja.
Agizo hilo la Waziri Mchengerwa limekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya Waganga Wafawidhi kuwa wamekuwa wakiondolewa kwenye nafasi zao kwa hila, kinyume na sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma.