Marie Louise Eta aandika historia Ulaya
Marie Louise Eta ameandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kufundisha timu ya wanaume katika ligi kuu za Ulaya, baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Union Berlin inayoshiriki Bundesliga hadi mwisho wa msimu.
Eta mwenye umri wa miaka 34, anachukua nafasi ya Steffen Baumgart ambaye aliondoka mwishoni mwa wiki kufuatia kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya timu ya mkiani Heidenheim.
Kwa sasa Union Berlin ipo katika hali tete, ikiwa na ushindi wa mechi mbili pekee kati ya 14 zilizopita, na bado haijajihakikishia kubaki ligi kuu ikiwa juu kwa pointi sita tu kutoka eneo la kushuka daraja.

Siyo mara ya kwanza kwake
Kwa Eta, jukumu hili si geni kabisa, kwani mwaka 2023, aliweka historia kwa kuwa kocha msaidizi wa kwanza mwanamke katika Bundesliga akiwa na Union Berlin, na pia akashiriki kuweka rekodi katika UEFA Champions League.
Baadaye, Machi 2025, aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana chini ya miaka 19 ya wanaume kabla ya kupandishwa tena kwa jukumu hili la muda mfupi kabla ya kurejea kuinoa timu ya wanawake ya Union Berlin.
“Nina furaha kubwa klabu kuniamini na kunikabidhi jukumu hili lenye changamoto,” alisema Eta kupitia taarifa ya klabu.
“Moja ya nguvu kubwa ya Union imekuwa ni mshikamano katika nyakati ngumu, na ninaamini kabisa tutapata pointi muhimu.
Kutoka uwanjani hadi benchi la ufundi
Kabla ya kuwa kocha, Eta alikuwa mchezaji mahiri ambapo alitwaa ubingwa wa Ujerumani mwaka 2009 na UEFA Women’s Champions League mwaka 2010 akiwa na klabu ya Turbine Potsdam.
Alistaafu soka mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 26, kisha akaingia moja kwa moja kwenye ukocha akiwa na Werder Bremen, akisimamia timu za akademi na pia kuwa kocha msaidizi wa timu za taifa za vijana.
Mwaka 2023 alipata leseni ya juu kabisa ya ukocha na kueleza: “Nimezoea kupiga hatua moja baada ya nyingine.
Naweza kujiona nikifanya mambo mengi kuinoa timu ya taifa ya vijana, kuwa msaidizi kwenye ligi za wanaume, au hata kufundisha timu za wanawake au vijana wa kiume.
”Upekee wake kwenye soka la wanaume
Eta anasema hajawahi kuona changamoto kuwa mwanamke katika mazingira yanayotawaliwa na wanaume.“Ninatambua hilo linanipa upekee fulani.
Wapo wanaoliona kama jambo la kipekee, lakini nimekua nikicheza na wavulana tangu utotoni na pia kufundisha kwenye akademi.
Sipendi kutazamwa kama kesi maalum,” alisisitiza. Uongozi wa Union Berlin una imani kubwa naye, huku mkuu wa soka la kulipwa, Horst Heldt akisema anafurahia Eta kukubali jukumu hilo.

Wanawake wengine waliowahi kufundisha wanaume
Ingawa Eta ameweka historia katika Bundesliga, si mwanamke wa kwanza kufundisha timu za wanaume barani Ulaya.
Miongoni mwa waliomtangulia ni Carolina Morace aliyewahi kuinoa klabu ya Viterbese mwaka 1999, pamoja na Sabrina Wittmann anayefundisha Ingolstadt tangu 2024.
Pia yupo Renate Blindheim ambaye amekuwa kocha wa klabu ya Sotra nchini Norway tangu 2020.
FIFA yasukuma usawa wa kijinsia
Uteuzi wa Eta unakuja wakati FIFA ikichukua hatua kuongeza nafasi kwa wanawake kwenye ukocha.
Shirika hilo limeelekeza kuwa timu za wanawake lazima ziwe na kocha mkuu au msaidizi mwanamke ili kushiriki mashindano yake, ikiwemo FIFA Women’s World Cup 2027.
Afisa mkuu wa soka wa FIFA, Jill Ellis alisema: “Bado idadi ya wanawake kwenye ukocha ni ndogo. Tunahitaji kuongeza juhudi kwa kufungua njia zaidi, kupanua fursa, na kuongeza uwakilishi wao uwanjani.”
