Kanisa Katoliki limewahimiza waamini kutumia fursa ya kupokea Rehema Kamili wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni, yatakayofanyika Oktoba 18, mwaka 2026.
Wito huo umetolewa na Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume, Penitenzieria Apostolica, kupitia waraka unaowahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa.
Rehema Kamili ni msamaha wa adhabu za muda mbele ya Mungu kwa ajili ya dhambi ambazo hatia yake tayari imesamehewa. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, mwamini anaweza kupata rehema hii kwa kutimiza masharti yaliyowekwa na Kanisa, kwa kutumia hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na watakatifu wake.
Masharti hayo yanajumuisha kuwa na nia ya kweli ya toba na wongofu wa ndani, kupokea Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu, kusali kwa nia ya Baba Mtakatifu Leo wa Kumi na Nne, pamoja na kutembelea kanisa au kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya tukio hilo, kwa kuzingatia masharti yanayotumika.
Rehema Kamili inaweza kupatikana kwa ajili ya mwamini mwenyewe au kwa ajili ya marehemu, kulingana na masharti ya Kanisa.
Katika ujumbe wake wa video, Baba Mtakatifu Leo wa Kumi na Nne amesema maadhimisho ya miaka 100 ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni ni fursa ya kumshukuru Mungu na kumkumbuka Papa Pio wa Kumi na Moja, aliyeanzisha maadhimisho hayo.
Baba Mtakatifu amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uelewa wa waamini kuhusu ukuu wa utume wa kimisionari katika kila Jimbo na Parokia, pamoja na kuhimiza sala za dhati kwa ajili ya uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mwanadamu kiroho na kimwili.
Aidha, amehimiza kuendeleza hamasa ya miito ya kimisionari na kutoa msaada kwa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, yanayojulikana kwa kifupi kama PMS.
Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume limewataka waamini kuhamasishana na kujiandaa ipasavyo ili kutumia fursa hiyo ya kupokea Rehema Kamili, huku wakitafakari wajibu wao katika kueneza Injili ya Yesu Kristo kwa njia ya sala, ushuhuda wa maisha ya Kikristo na kusaidia shughuli za kimisionari.
Maadhimisho ya miaka 100 ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni yanatarajiwa kuwa fursa ya kuimarisha imani na mshikamano wa waamini, pamoja na kufufua ari ya kushiriki katika utume wa Kanisa duniani kote.
