Na Shafiru Yusuph- Muleba, KAGERA
Mamlaka ya Serikali za Mitaa kanda ya ziwa (LVRLAC) Tanzania imefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na kupongeza Ujenzi wa Soko kuu la Muleba Mjini ambalo linagharimu shilingi bilioni tatu kwa kuongeza mapato na kuinua uchumi wa wananchi.
Mwenyekiti wa LVRLAC Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Magongo Justus amesema ziara hiyo imelenga kuwapa wajumbe nafasi ya kujifunza na kujionea hatua zinazopigwa na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa LVRLAC Tanzania na Meya wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Bw. Mataluma Kaniki amesema ujenzi wa soko hilo utakuwa mfano wa kuigwa kwa kubuni miradi mikubwa ya kimkakati ambayo itaongeza mapato ya ndani na kuinua uchumi wa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndugu Isaya Mbenje akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Soko la Kisasa la Muleba Mjini (Kariakoo) amesema mradi huo unaojengwa kwa mapato ya ndani unatarajiwa kuanza kutumika kwa awamu ya kwanza mwezi Juni 2026 huku awamu ya pili pamoja na eneo lote la soko ikikamilika Septemba 2026.
Aidha, Kamati Tendaji ya LVRLAC Tanzania inajumuisha wenyeviti wa halmashauri, madiwani pamoja na wataalamu kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo imefanya kikao chake cha kwanza cha siku mbili mjini Bukoba kabla ya kufanya ziara hiyo wilayani Muleba.

