Na Clement Shawishi – Geita
Serikali imeagiza Vyama vya Ushirika Mkoani Geita kuwajibika kulipa kwa wakati madeni vinayodaiwa na wakulima na Kampuni mbalimbali zinazofanya kazi na Vyama hivyo.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Geita kwenye Kongamano la Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Geita lililofanyika Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro.

Komba amesema kuwa ucheleweshaji wa malipo kwa wadau wa Ushirika kunadhoofisha jitihada walizonazo katika uzalishaji malighafi na bidhaa na kwamba tabia hiyo siyo ya kufumbia macho
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia Kampuni zote zilizoshindwa kulipa madeni ya Vyama vya Msingi vya Kilimo na Masoko (AMCOS)
Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika Geita (GCU) Bw, Kamuli Ngoya kwa niaba ya Viongozi wengine wa Vyama vya Ushirika ameahidi kufanyia kazi maelekezo hayo ili kuwaepushia hasara wadau wa Ushirika

Mjumbe wa Bodi ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Geita Bi, Mariam Sharif amehimiza Umoja na ushirikiano miongoni mwa wanachama katika Vyama vya Ushirika kurahisisha utatuzi wa changamoto ndani ya Vyama hivyo.
