Na Clement Shawishi – GEITA
Wananchi Mkoani Geita wamekumbushwa kutimiza wajibu wao wa kisheria kuthamini na kutunza Wanyama kwa masilahi ya Taifa kiuchumi na mtu mmoja mmoja
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kwenye maadhimisho ya siku ya Punda duniani ambayo kitaifa yamefanyika Kata ya Mgusu Mkoani Geita mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mkuu huyo wa Wilaya amehimiza Mashirika yanayohusika na Ustawi wa Wanyama, Serikali za mitaa na wadau wengine kuhakikisha yanafuatilia na kuwachukulia hatua za kisheria wanaovunja haki za Wanyama
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Shaban Tozzo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, amesema Serikali imeridhia maadhimisho hayo kufanyika Geita kutokana na Punda kusaidia sana shughuli za uchimbaji
Mwakilishi wa Taasisi zisizo za kiserikali zinazohusika na Uhifadhi wa Wanyama Bw, Evarist Maguo amesema kutokana na uelewa mdogo wa Wananchi kuhusu haki za Wanyama Taasisi hizo zinaendelea kutoa chanjo, Elimu na kufanya utafiti zaidi kuhusu Wanyama.
Maadhimisho ya siku ya Punda duniani Mei 8 ya kila mwaka ni matokeo ya utekelezaji wa Tamko la Azimio la Umoja wa Nchi huru Afrika kwenye mkutano uliofanyika Dar es salaam Oktoba 2022, Kaulimbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni “Kulinda Punda wa Afrika ni Jukumu letu site”
