Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amezitaka mamlaka zinazoshughulikia masuala ya kibiashara kati ya Tanzania na Burundi kushughulikia na kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru na forodha vinavyokwamisha ufanisi wa kibiashara baina ya mataifa hayo mawili.
Balozi Sirro ametoa kauli hiyo wakati akifungua maonesho ya pamoja ya biashara yanayofanyika jijini Bujumbura nchini Burundi alipomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara.
Amevitaja baadhi ya vikwazo hivyo kuwa ni uwepo wa taratibu zinazochukua muda mrefu maeneo ya mipakani, kanuni zinazobadilika mara kwa mara, kutofautiana kwa viwango vya ushuru sambamba na utekelezaji kanuni unaobadilika mara kwa mara.
Amesema njia bora ya kukabiliana na changamoto hiyo ni kufanyika kwa vikao vya mara kwa mara vinavyojumuisha pande zote mbili ambazo ni Tanzania na Burundi ili kuwaondolea kero wananchi.
