Katika jitihada za kuongeza uzalishaji wa mpunga wenye tija, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Research Institute – TARI) imewapatia mafunzo wakulima wa kijiji cha Lunwa, Kata ya Igurusi wilayani Mbarali mkoani Mbeya kuhusu matumizi ya mbegu bora na kanuni za kilimo bora.
Mtafiti kutoka TARI Kituo cha Dakawa mkoani Morogoro, Barnabas Sitta, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wakulima kutumia mbegu sahihi na teknolojia za kisasa za kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa mazao na kuinua kipato cha wakulima katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Igurusi, Pius John, amesema elimu hiyo itawasaidia wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kuzingatia kanuni bora za uzalishaji zitakazoongeza tija katika kilimo cha mpunga na kupunguza hasara zinazotokana na matumizi ya mbegu zisizo bora.
Baadhi ya wakulima walioshiriki mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa wa kuchagua mbegu bora na kutumia mbinu sahihi za kilimo, hatua wanayoamini itachangia kuongeza mavuno na kuimarisha kipato chao kupitia kilimo cha mpunga.
