Msanii wa Hip Hop nchini, Witness Mwaijaga Sigbjorn maarufu kama Witnesz, ameteuliwa kuwa Balozi wa Muziki wa Tanzania na taasisi ya 54 African Mamas, hatua inayotambua mchango wake katika kukuza muziki na kuhamasisha maendeleo ya wanawake ndani ya sekta ya ubunifu barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, uteuzi huo unampa jukumu la kuiwakilisha Tanzania katika shughuli mbalimbali za kikanda na kimataifa zinazohusu muziki, utamaduni na uwezeshaji wa wanawake, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiutamaduni kati ya mataifa ya Afrika.
Aidha, Witnesz anatarajiwa kushiriki katika mkutano na tamasha la African Women in Music Summit and Concert litakalofanyika nchini Afrika Kusini kuanzia Juni 21 hadi 28, 2026, ambapo wasanii, watunga sera na wadau wa sekta ya muziki kutoka nchi mbalimbali za Afrika watakutana kujadili maendeleo ya tasnia hiyo.
Akizungumzia uteuzi huo, Witnesz amesema ameupokea kwa heshima kubwa na yuko tayari kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu, huku akiahidi kuitangaza Tanzania na kuchangia maendeleo ya muziki wa Afrika kwa ujumla.
