Clement Shawishi- GEITA
Afisa Elimu Kata ya Nyarugusu Wilayani Geita Bw. Robert Roth amewasihi wazazi na Bodi za shule kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utatuzi wa vikwazo kwa wanafunzi shuleni ili kufikia lengo la kuinua sekta ya elimu.
Bw. Roth amesema hayo wakati akipokea ufadhili wa Vifaa vya masomo kwa wanafunzi 101 wa kidato cha Kwanza katika shule 3 za sekondari uliotolewa na Asante Africa Foundation kwa ushirikiano na Mgodi wa Mwamba Mining
Amewaomba wazazi na walezi kuwajibika kwa nafasi yao kwa kufuatilia mienendo ya watoto kabla, wakati na baada ya masomo ili kuhakikisha msaada wanaopewa unachochea maendeleo ya watoto kitaaluma.
Meneja wa Asante Africa Foundation Bw. Florence Thomas amebainisha kuwa wanafunzi waliofikiwa ni kutoka shule ya sekondari Dhahabu, Evarist na Lwamugasa dhamira kuu ikiwa ni kuongeza ufanisi wa sera ya elimu bure.

Meneja wa Mgodi wa Mwamba Mining Bw. Calvin Habil amesema kampuni hiyo inashiriki katika mradi huo kutekeleza sera yake isemayo madini yaliyopo chini ya ardhi yawanufaishe watu waliopo juu ya ardhi
Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu Bw. Lusekelo Mwaikenda amepongeza wadau kwa ufadhili huo na kusisitiza kuwa Ofisi yake imeweka mipango thabiti kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekatisha masomo
Ufadhili huo unahusisha msaada wa sare za shule, madaftari, mabegi pamoja na vifaa vya usafi na baiskeli kwaajiri ya usafiri kwa wanafunzi wanaotoka mbali hususani wa kidato cha kwanza kutoka familia zenye kipato cha chini.
