Na Samwel Masunzu – Kibondo, KIGOMA
Wajasiriamali na wanaofanyabiashara kwenye soko la stendi ya zamani kata ya Kibondo mjini wilayani Kibondo mkoani Kigoma wamelazimika kutumia vyoo vya watu binafsi majumbani baada ya choo na bafu vya soko hilo kutitia.
Wakizungumza na Redio Kwizera leo Mei 12 wamesema jengo la choo na bafu vimefungwa kwa matumizi na kubomolewa na maafisa wa halmashauri ili kuepusha madhara hali inayowalazimu kutumia vyoo vya watu majumbani.

Wamesema wanaomba serikali kuvijenga kwa haraka ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo mlipuko wa magonjwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo Bw. Stephen Janks akizungumzia suala hilo kupitia kikao cha baraza la madiwani mwishoni mwa wiki iliyopita alisema baada ya dharura walituma wataalamu ambao waliweka dawa ya ‘Chlorine’ kuzuia hatari kwa wakazi wa eneo hilo.
Janks amesema walilazimika kufunga huduma ya choo na kwa sasa wajasiriamali watatumia choo kilichopo eneo la soko lililokuwepo soko la samaki wakati ambao utaratibu wa choo cha stendi ya zamani ukiendelea.
