Na Enock Yoronimo- Bukoba, KAGERA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatina Hussein Laay, amekabidhi pikipiki kwa watumishi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika kata za Rukoma, Mgajwale, Izimbya, Bujugo na Katoro, ili kurahisisha na kuboresha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi za Halmashauri hiyo, Bi. Laay amewataka watumishi hao kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, kwa kuzingatia umuhimu wake katika kuleta maendeleo ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo, Felster Shayo, amesema fedha zilizotumika kununua pikipiki tano zimetokana na marejesho ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri hiyo.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa wakati, ufanisi na weledi, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
