Rais William Ruto ametangaza hatua za kupunguza makali ya gharama ya maisha baada ya wiki ya maandamano na mgomo wa sekta ya uchukuzi uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta nchini Kenya.
Katika hotuba yake kwa taifa Ijumaa, Rais Ruto alisema Serikali imekubaliana kupunguza bei ya dizeli kwa shilingi 10 kwa lita kuanzia mzunguko ujao wa bei za mafuta wa mwezi Juni hadi Julai, hatua aliyosema inalenga kupunguza mzigo kwa wananchi na wafanyabiashara waliokuwa wakikabiliwa na gharama kubwa za usafiri na bidhaa muhimu.
Rais pia alieleza kuwa Serikali pia imeweka mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea bila usumbufu huku akisisitiza kuwa mgogoro wa bei ya mafuta umetokana na changamoto za Kimataifa za usambazaji wa nishati kufuatia mvutano wa Mashariki ya Kati.
Hotuba hiyo imejiri siku chache baada ya mgomo wa kitaifa wa wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma kusababisha usumbufu mkubwa wa usafiri katika maeneo mbalimbali nchini huku maandamano yakisababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.
Wakati huo huo, viongozi wa sekta ya uchukuzi wametangaza kufutilia mbali mgomo huo kwa muda wa wiki moja baada ya mazungumzo na Serikali, na kuwataka wahudumu kurejea kazini huku mazungumzo zaidi yakiendelea kuhusu gharama ya mafuta.
Rais Ruto aliwataka Wakenya kudumisha amani na kutoa nafasi kwa Serikali kushughulikia changamoto hiyo, akiahidi kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kulinda uchumi na maisha ya wananchi.
