Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za kikomo za bidhaa za mafuta zitakazoanza kutumika kuanzia leo, Juni 3, 2026.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Gerald Maganga, bei ya petroli katika Jiji la Dar es salaam imeshuka kwa shilingi 29 kwa lita na sasa itauzwa kwa shilingi 4,086 kutoka shilingi 4,115 ya mwezi uliopita.
Kwa upande wa dizeli, bei imeongezeka kwa shilingi 85 kwa lita licha ya kuwekewa ruzuku ya shilingi 534 kwa lita. Baada ya ruzuku hiyo, dizeli inayopitia Bandari ya Dar es Salaam itauzwa kwa shilingi 4,333 kwa lita kutoka shilingi 4,248 iliyokuwapo mwezi Mei 2026.
