Waumini wa Kanisa Katoliki duniani kote kesho wanaadhimisha Jumapili ya Ekaristi Takatifu, siku maalum inayowakumbusha nafasi ya sakramenti hiyo katika kuimarisha imani, kuunganisha waamini na Kristo, na kuwapatia neema ya kiroho katika maisha yao ya kila siku.
Katika maadhimisho hayo, waumini wanahimizwa kutafakari kwa kina zawadi ya Ekaristi Takatifu ambayo Kanisa linaifundisha kuwa ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo ambapo Kupitia Ekaristi, waamini hupokea Mwili na Damu ya Kristo na hivyo kuimarisha ushirika wao na Mungu pamoja na ndugu zao katika imani.
Akizungumza na Radio Kwizera kuelekea maadhimisho hayo, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Ngara Mjini, Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Padre Vedasto James Ademba amesema Ekaristi Takatifu ni ishara ya uponyaji kwa waamini wote wanaoikaribia kwa imani ya kweli.
Padre Ademba amesema Kristo anaendelea kujitoa kwa watu wake kupitia Ekaristi na kwamba kila muumini anapaswa kuwa na imani thabiti katika sakramenti hiyo ili aweze kupokea neema na uponyaji wa kiroho unaotokana nayo.
Amesema wengi hutafuta uponyaji katika maeneo mbalimbali, lakini nguvu ya uponyaji wa Kristo ipo katika Ekaristi Takatifu, ambapo waamini wanakutana naye kwa namna ya kipekee, Amesisitiza kuwa imani ndiyo ufunguo wa kupokea matunda ya sakramenti hiyo.
Aidha amesema Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya sakramenti zote za Kanisa na ndiyo kilele cha ibada na uabudu wote wa maisha ya Kikristo na kupitia Ekaristi, waamini hupata nguvu ya kuishi Injili, kuvumilia changamoto za maisha na kuendelea kushuhudia upendo wa Mungu katika jamii.
Maadhimisho ya Jumapili ya Ekaristi Takatifu pia yanatoa fursa kwa waamini kutambua uwepo halisi wa Kristo katika Sakramenti ya Altare na kuhuisha heshima, ibada na upendo wao kwa Ekaristi ambayo ni kitovu cha maisha ya Kanisa.
Kanisa linaendelea kuwakaribisha waamini wote kushiriki kikamilifu katika adhimisho hilo, likikumbusha kuwa kila anayemkaribia Kristo kwa imani hupata nguvu mpya, faraja ya moyo na neema ya kuendelea kutembea katika njia ya wokovu.
