Papa Leo wa XIV ameonesha masikitiko makubwa kufuatia kuuawa kwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Quelimane na Msimamizi wa Kitume wa Beira, Askofu Osório Citora Afonso, aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa risasi nchini Msumbiji.
Kwa mujibu wa ujumbe uliotolewa na Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu kupitia chaneli yake ya Telegram, Papa amesema amepokea kwa huzuni taarifa za tukio hilo la vurugu na kuungana katika sala na waamini wa Majimbo ya Quelimane na Beira pamoja na wananchi wote wa Msumbiji katika kipindi hiki cha maombolezo.
Taarifa hiyo, iliyotolewa na Msemaji wa Kiti Kitakatifu, Matteo Bruni, imeeleza kuwa Papa amemwomba Mwenyezi Mungu awafariji wote walioathirika na tukio hilo na kuwalinda watu dhidi ya vitendo vya vurugu.
Askofu Osório Citora Afonso alipatikana amefariki dunia Juni 6, 2026 katika makazi ya maaskofu yaliyopo Quelimane. Taarifa kutoka kwa vyombo vya usalama na Baraza la Maaskofu wa Msumbiji zinaeleza kuwa alipigwa risasi kadhaa kifuani na eneo la moyo, huku sababu za tukio hilo zikiendelea kuchunguzwa na mamlaka husika.
Naye Rais wa Baraza la Maaskofu wa Msumbiji, Inácio Saúre, ametoa wito kwa waamini kuendelea kuwa na imani na mshikamano wa kindugu katika kipindi hiki kigumu.
Wakati huo huo, Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, ametoa salamu za rambirambi akieleza kuwa kifo cha askofu huyo ni pigo kubwa si kwa Kanisa Katoliki pekee bali pia kwa taifa zima la Msumbiji.
Marehemu Askofu Osório Citora Afonso pia aliwahi kulitumikia Kanisa katika ngazi mbalimbali za kimataifa, ikiwemo kuwa afisa wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji kati ya mwaka 2017 na 2023.
