Papa Leo XIV amewasili jijini Barcelona nchini Hispania leo Jumanne Juni 9, 2026, ikiwa ni hatua ya pili ya Ziara yake ya Kitume nchini humo iliyoanza Juni 6 mwaka huu.
Siku chache kabla ya kuwasili kwake, mamlaka za jiji hilo zilikuwa zikiendelea na maandalizi mbalimbali ikiwemo kusafisha mitaa, kuboresha miundombinu ya barabara na kuandaa maeneo yatakayotumika katika shughuli za kipapa. Wakati huo huo, Kanisa Katoliki limeendelea kuandaa kumbi na maeneo ya ibada kwa ajili ya mapokezi ya Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani.
Ziara hiyo pia imebeba uzito wa kihistoria kutokana na hadhi ya Barcelona kama Mji Mkuu wa Dunia wa Usanifu wa Majengo kwa mwaka 2026 uliotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO. Miongoni mwa vivutio vikubwa vya jiji hilo ni Basilika ya Familia Takatifu, maarufu kama Sagrada Familia, iliyobuniwa na mbunifu mashuhuri Antoni Gaudí. Mwaka huu Barcelona pia inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 tangu kifo cha mbunifu huyo.
Mbali na kushiriki katika maadhimisho yanayohusiana na urithi wa Gaudí, Papa Leo XIV anatarajiwa kukutana na waamini na viongozi wa Kanisa pamoja na kutembelea parokia inayohudumia wahamiaji jijini Barcelona.
Parokia hiyo inaendeshwa na Jumuiya ya Waagostino yenye mapadre wanne pekee katika jiji hilo, wakiwemo wawili kutoka Tanzania na wawili kutoka Ufilipino. Kupitia huduma zao, mapadre hao wamekuwa wakitoa msaada wa kiroho na kijamii kwa wahamiaji wanaoishi jijini Barcelona, jambo linalotarajiwa kupata msukumo zaidi kupitia ziara ya Papa Leo XIV.
