Michael Mpunije- Kasulu, Kigoma
KASULU: Mwenge wa Uhuru 2026 wiki hii ukiwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma meweka Jiwe la Msingi katika ofisi ya mtendaji wa mtaa wa mgandazi Kata ya Murufiti.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Mtendaji wa Mtaa wa Mugandazi, Mariamu Jangama, amesema ujenzi wa ofisi hiyo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 42 na umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya wananchi, Halmashauri na wadau wa maendeleo.
Amesema wananchi wamechangia zaidi ya shilingi mil 4, huku Halmashauri ikitoa shilingi milioni 32 kutoka mapato ya ndani wakati huo wadau mbalimbali wa maendeleo wakichangia vifaa na fedha vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni sita.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako, amewataka wananchi wa Mtaa wa Mugandazi kuendelea kushikamana, kudumisha amani na kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amesema Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia upatikanaji wa Huduma Bora kwa wananchi.
