Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema linafanya uratibu kwa karibu na serikali ya Kenya kukabiliana na matishio ya kiafya yanayohusiana na msimu wa mvua za El Nino.
Akizungumza jijini Nairobi kabla ya msimu wa mvua wa Oktoba – Desemba, Mwakilishi wa WHO nchini Kenya, Neema Kimambo amesema tathmini endelevu za matishio zitatoa mwongozo kwa mamlaka za afya katika kutambua matishio.
Aidha amesema tathimini hiyo pia itasaidia kuimarisha utayari wa mwitikio dhidi ya mafuriko na milipuko ya magonjwa inayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa. Katika kukabiliana na hali hiyo, Wizara ya Afya nchini Kenya imeanzisha Mpango wa Sekta ya Afya Kukabiliana na El Nino, ili kutoa mwongozo wa juhudi za kitaifa za utayari na mwitikio wa dharura.
