Wafugaji nchini wanatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato kupitia Mradi wa Tuzo Shindani za Watoa Huduma kwa Ajili ya Tasnia Himilivu ya Maziwa, unaolenga kuwahamasisha kutumia mbinu bora za ufugaji, malisho bora na huduma zenye tija.
Mradi huo unaotekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Morogoro, unalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato cha wafugaji pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa katika tasnia hiyo.
Akizindua mradi huo unaofadhiliwa na Heifer International, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, alisema tuzo hizo ni sehemu ya jitihada za kuongeza tija katika ufugaji na uzalishaji wa maziwa kwa kuwahamasisha wafugaji kutumia teknolojia na mbinu bora za ufugaji.
Alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya mbegu bora za malisho, uzalishaji wa malisho ya kutosha na matumizi ya teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji wa mifugo.
