Enock Yoronimo- Ngara, Kagera.
Kamati ya Madiwani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera imekiagiza Chama cha Ushirika cha Wakulima cha Ngara Farmers kuhakikisha kinawalipa wakulima fedha zao za mauzo ya kahawa zilizolimbikizwa kwa muda mrefu.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Wilbard Bambara, wakati wa kikao cha dharura kati ya kamati hiyo na wajumbe wa Bodi ya Ngara Farmers, kilicholenga kutafuta suluhisho la changamoto ya kuchelewa kwa malipo ya wakulima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Solomon Kimilike, amesema Ngara Farmers ilitakiwa kulipa ushuru wa Tsh milioni 185 kwa Halmashauri, lakini hadi sasa imelipa milioni 79.5 pekee na hivyo kubakiwa na deni la zaidi ya milioni 100.

Wakati huo huo, baadhi ya madiwani wameeleza kuwa viongozi wa chama hicho wamekuwa wakikiuka sheria na taratibu za ushirika, jambo ambalo limekuwa likisababisha usumbufu na hasara kwa wakulima wa kahawa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ngara Farmers, Justa Pendo Leonard, amesema kuchelewa kwa malipo ya wakulima kunatokana na ucheleweshaji wa fedha kutoka Bodi ya Kahawa.
Hata hivyo, Kamati ya Madiwani imeitoa onyo kali kwa Bodi ya Ngara Farmers endapo Kuna ubadhirifu katika uendeshaji wa chama hicho, na kuahidi kuchukua hatua za kuwaondoa viongozi watakaoshindwa kujirekebisha.
