Bei ya mafuta ghafi duniani imezidi kupanda na kuvuka dola 110 (Sh283,000) kwa pipa katika kipindi cha miaka minne huku masoko ya hisa yakishuka, kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi wa kukatizwa kwa usafirishaji wa nishati kupitia Strait of Hormuz kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Wasiwasi huo umeongezeka wakati Iran ikimtangaza Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi Mkuu mpya wa taifa hilo baada ya kifo cha baba yake Ali Khamenei.
Mwisho wa wiki, Marekani na Israel zilianzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga katika maeneo mbalimbali ya Iran, yakilenga miundombinu kadhaa ikiwemo maghala ya mafuta, jambo lililoongeza hofu ya kutokea kwa usumbufu mkubwa katika usambazaji wa nishati kutoka Mashariki ya Kati.
Akizungumzia ongezeko hilo, Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kupanda kwa bei kwa muda mfupi ni gharama ndogo ya kulipa ili kuondoa kile alichokiita tishio la nyuklia kutoka Iran.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kuanzia Machi 4, 2026, bei ya rejareja ya petroli jijini Dar es Salaam ilionesha kuongezeka hadi Sh2,864 kwa lita kutoka Sh2,788 ya Februari, ikiwa ni ongezeko la Sh76.
Dizeli ilipanda kwa kasi zaidi ikiwa na ongezeko la Sh157, ambapo inauzwa Sh2,858 kutoka Sh2,701, huku mafuta ya taa yakiongezeka kwa Sh186 ambapo itauzwa Sh2,932 kutoka Sh2,746 pamoja na maeneo mengine pia kukiwa na ongezeko la bei ya bidhaa hiyo.
