Baba Mtakatifu Papa Leo XIV leo Alhamisi Juni 11, 2026 ameondoka jijini Barcelona kuelekea Las Palmas de Gran Canaria katika hatua ya tatu ya ziara yake ya kitume nchini Hispania.
Papa ameondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Josep Tarradellas Barcelona-El Prat majira ya saa 2:45 asubuhi, baada ya kuhitimisha shughuli zake jijini Barcelona ambapo Juni 10 aliadhimisha Misa Takatifu katika Basilika ya Familia Takatifu na kuzindua mnara wa Kanisa hilo maarufu.
Katika kituo chake kipya cha Las Palmas de Gran Canaria, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuanza ratiba yake kwa kukutana na wadau mbalimbali kujadili hali halisi ya mapokezi na huduma kwa wahamiaji, suala ambalo limekuwa miongoni mwa ajenda muhimu za Kanisa Katoliki duniani.
Asubuhi kabla ya kuondoka, Papa Leo XIV aliondoka makazi ya Askofu Mkuu wa Barcelona kuelekea uwanja wa ndege ambako alipokelewa na viongozi wa eneo hilo kabla ya kupanda ndege ya Iberia A320 iliyompeleka katika Kisiwa cha Gran Canaria.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Papa atapokelewa na mamlaka za eneo la Gran Canaria mara baada ya kuwasili, kabla ya kushiriki mkutano maalum katika ukumbi wa wageni mashuhuri.
Ziara ya Papa katika Visiwa vya Canary, ikiwemo Las Palmas de Gran Canaria na Santa Cruz de Tenerife, inahitimisha ziara yake ya nne ya kitume nchini Hispania iliyoanza rasmi Juni 6 mwaka huu.
