Baadhi ya wakulima wa zao la kahawa wilayani Karagwe Mkoani Kagera wamelalamikia kukosa miche ya zao hilo katika msimu wa upandaji na kwamba hali hiyo inakwamisha uzalishaji.
Wameeleza hayo wakati wakizungumza na Radio Kwizera ambapo wamesema wamekuwa wakianda mashamba kwa kutumia gharama kubwa na matokeo yake hukosa miche kutoka halmashauri na wadau walioteuliwa kutoa miche hiyo.
Sud Abubakiri na Leonard Ntindamanyire wamesema halmashauri ya wilaya ya Karagwe inatakiwa kuweka utaratibu mzuri wa kumfikia mkulima wa chini katika upatikanaji wa miche
Naye Mkuu wa wilaya ya Karagwe Bw. Julius Laizer kupitia baraza la madiwani amekiri halmashauri kutofanya vizuri na kuahidi msimu ujao atahakikisha halmashauri inakuwa na kitalu kinachojitegemea.
