Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amesema ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, hadi kufikia mwezi Desemba 2025 Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kuanzisha kongani 36 katika mikoa 16 nchini ambapo kati ya hizo, kongani sita zipo katika hatua ya ujenzi na baadhi ya viwanda ndani ya kongani hizo tayari vimeanza uzalishaji.
Amesema, mathalani, kongani ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani na Kongani ya Kilimanjaro iliyopo Kigamboni, kila moja ina viwanda vinne vilivyoanza uzalishaji.
Aidha, Londo amesema Serikali imeanza kutekeleza mpango maalumu wa miaka sita wa kuendeleza viwanda nchini ambapo kupitia mpango huo, kongani zipatazo 52 (kongani 2 kwa kila mkoa) zitajengwa.
Londo amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mahonda mkoani Kaskazini B, Zanzibar, Othman Suleiman aliyehoji ipi mikakati ya Serikali ya kuongeza viwanda nchini ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
