Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema ushiriki wa Tanzania kwenye mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) upo kwenye biashara ya kusafirisha mafuta ghafi tu (transit nation) kutoka Kabaale Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga na baadaye kupelekwa kwenye masoko ya kimataifa.
Amesema mikataba ya mauzo ya mafuta hayo imeingiwa kati ya wabia wa mkondo wa juu nchini Uganda (upstreamers) ambao ni Serikali ya Uganda na makampuni ya kimataifa (TotalEnergies kutoka Ufaransa na CNOOC kutoka China) kwa kuzingatia vigezo vya usanifu wa kitaalamu na uwezo wa uzalishaji wa visima.
Aidha, Makamba amesema ifahamike kuwa kwenye biashara hiyo tayari mikataba ya mauzo ya mafuta hayo imeshaingiwa kati ya wabia wa mkondo wa juu (upstreamers) na wanunuzi (masoko ya kimataifa).
Makamba ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Bahi mkoani Dodoma, Kenneth Nollo aliyetaka kujua, Serikali ina mpango gani wa kuanza kusafirisha mafuta ghafi yanayotoka Uganda kupitia bomba hilo.
