Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, ametembelea na kuingia katika msikiti mkubwa zaidi nchini Algeria, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya kuimarisha mahusiano ya kidini.
Papa ametembelea Djamaa el Djazair jijini Algiers, msikiti wenye uwezo wa kuchukua zaidi ya waumini 100,000 kwa wakati mmoja, ambapo alipokelewa na viongozi wa Kiislamu na kuzunguka eneo hilo kwa kufuata taratibu za ibada.
Akiwa ndani ya msikiti huo, amesimama kwa muda wa utulivu na kufanya sala fupi, akisisitiza umuhimu wa amani, kuheshimiana na mshikamano kati ya Wakristo na Waislamu.
Ziara hiyo ni sehemu ya ziara yake ya kwanza barani Afrika inayojumuisha pia Cameroon, Angola na Equatorial Guinea, ikiwa na lengo la kuhimiza maelewano ya kidini na maendeleo endelevu.
Hatua hiyo imeelezwa kama tukio la kihistoria linaloimarisha mazungumzo ya kidini na kuhamasisha jamii kuishi kwa amani licha ya tofauti za kiimani.
