Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linasikitika kutangaza kifo cha Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, kilichotokea leo Aprili 14, 2026 majira ya Saa 11:45 asubuhi kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa, BMH alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya dharura.
Askofu Mfumbusa anatarajiwa kuzikwa Jumatano Aprili 22, 2026 Jimboni Kondoa.
Itakumbukwa kwamba, Aprili 9, 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV alikuwa amemteua Askofu Bernardin Francis Mfumbusa, Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, “Pan African Episcopal Conference For Social Communication, CEPACS,” kuwa ni Mjumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasilianiano ya Jamii.
Kanisa limempoteza Askofu na mtaalam mbobezi wa Mawasiliano ya Jamii.
Itakumbukwa kwamba, Hayati Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, alizaliwa Aprili 1, 1962 mjini Kondoa na ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64 tangu alipozaliwa.
Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi, Juni 14, 1992 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Askofu Matthias Joseph Isuja, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI Machi 12, 2011 akaanzisha Jimbo Katoliki la Kondoa na kumteuwa Askofu Bernardin Francis Mfumbusa kuwa Askofu wake wa kwanza, na hivyo kuwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mei 15, 2011, akisaidiana na Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza pamoja na Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp., wa Jimbo Katoliki la Zanzibar.
Askofu Bernardin Francis Mfumbusa amefariki dunia akiwa amelitumia Kanisa kama Padre kwa Miaka 33 na kama Askofu mwenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa miaka 14.
