Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kutimiza wajibu wao wa malezi na usimamizi bora wa watoto bila ubaguzi.
Askofu Kassala amesema kutokana na maendeleo ya kiuchumi na teknolojia, kwa sasa imeibuka jamii hatarishi ambapo baadhi ya watu hawapendi kuzaa huku wengine wakitelekeza watoto baada ya kuwazaa.
Askofu huyo ametoa rai hiyo leo Mei 29, 2026 wilayani Chato mkoani Geita, katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa mama mzazi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, Mama Sussana Ngolo.
Amesema wazazi wanapaswa kutambua kuwa licha ya sayansi kuruhusu utoaji salama wa mimba, kitendo hicho ni ukatili dhidi ya watoto kabla ya kuzaliwa na pia ni kinyume na mapenzi ya Mungu.
“Tunayo jamii ambayo ni hatarishi kwa sasa. Wapo wasiopenda kuzaa na ukifuatilia kwa undani si wote ni watoto yatima, mwingine utakuta anazaa na kumtelekeza mtoto. Tunao wengine waliotupwa siku ya kwanza ya maisha yao, ndiyo maana nyumba za kulelea watoto yatima zinaongezeka,” amesema Askofu Kassala.
Ameongeza kuwa licha ya Mama Sussana kuwa mtoto pekee katika familia yao, alijitahidi kuwalea watoto wote 15 aliojaliwa na hivyo taifa likapata viongozi na watu wachapakazi.
