Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Padre Dkt. Charles Kitima, amesema kuvurugwa na kuondolewa kwa dhana ya ushindani wa haki wa kisiasa ni miongoni mwa sababu kuu zilizoharibu mfumo wa uchaguzi na misingi ya demokrasia nchini.
Padre Kitima ameyasema hayo leo, Septemba 15, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani yaliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC.
Amesema tangu kipindi cha baada ya uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alisisitiza umuhimu wa kiongozi kupata uhalali wa kuongoza kupitia uchaguzi na ushindani wa haki unaotokana na wananchi.
Padre Kitima amesema mwaka 1962, Nyerere alisisitiza kuwa, licha ya Tanzania kupata uhuru Desemba 9, 1961, alipaswa kuchaguliwa na wananchi ili kupata uhalali wa kuongoza.
Kwa mujibu wa Padre Kitima, msingi huo uliweka wazi kwamba uongozi ni dhamana na mamlaka ya utawala yanatokana na wananchi.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Padre Kitima amesema kuongezeka kwa idadi ya wagombea urais hadi kufikia 17 hakukuashiria kukua kwa demokrasia, bali kulichangiwa na mbinu zilizolenga kuondoa ushindani halisi wa kisiasa.
Amesema hali hiyo ilianza kujitokeza tangu mwaka 2019 na 2020, huku akieleza kuwa kuvurugwa kwa ushindani wa kisiasa kulianza ndani ya vyama vya siasa kabla ya kufikia hatua ya uchaguzi mkuu.
Padre Kitima amesisitiza kuwa demokrasia ya kweli inahitaji kuwepo kwa ushindani wa haki na wa wazi, ili wananchi waweze kutumia mamlaka yao ya kuchagua viongozi kwa uhuru.
