Papa Leo XIV amewataka wafungwa wanaotumikia vifungo katika Kituo cha Wafungwa cha Brians 1 kilichopo nje kidogo ya jiji la Barcelona nchini Hispania kutokata tamaa, akisisitiza kuwa Mungu humpenda kila mtu bila ubaguzi na daima hutoa nafasi ya kuanza upya.
Papa ametoa ujumbe huo Juni 10 akiwa katika siku ya tano ya Ziara yake ya Kitume nchini Hispania alipowatembelea wafungwa wa kituo hicho kinachowahifadhi zaidi ya wanaume 1,000 na wanawake 150 wanaosubiri kesi mbalimbali mahakamani.
Akizungumza baada ya kusikiliza ushuhuda wa baadhi ya wafungwa pamoja na watumishi wa gereza, Baba Mtakatifu amesema kila mwanadamu ana thamani kubwa mbele za Mungu kwa kuwa ameumbwa na kupendwa naye, hivyo hakuna hali inayoweza kumfanya Mungu awaache watoto wake.
Papa Leo XIV amesema wafungwa wengi hubeba maumivu ya kutengana na familia zao pamoja na huzuni ya makosa yaliyopita, lakini amewakumbusha kuwa makosa hayo hayapaswi kuwa mwisho wa maisha yao.
Amesisitiza kuwa kwa kuamini neema ya Mungu na kuruhusu maisha yao kubadilishwa na upendo wake, wanaweza kupata nguvu ya kufanya maamuzi mapya na kujenga mustakabali bora zaidi.
Baba Mtakatifu pia amewahimiza wafungwa hao kumtengenezea Mungu nafasi mioyoni mwao na kuruhusu upendo wake kuwaongoza, akieleza kuwa hakuna kizuizi cha kimwili kinachoweza kuzuia mtu kufikia matumaini ambayo Mungu ameyaandaa kwa ajili yake.
Aidha amewataka kuendelea kuota ndoto za Mungu katika maisha yao, akisisitiza kuwa kuwa Mkristo hakumaanishi kutokosea kamwe, bali kuwa tayari kubadilika, kutubu, kusamehe na kupatanishwa.
Akihitimisha ujumbe wake, Papa Leo XIV amewakabidhi wafungwa hao katika maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Huruma, huku akiwaombea baraka na matumaini mapya katika maisha yao.
