Mtawa wa Shirika la Watumishi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kutoka Kenya, Sister Anne Ilia, amesema ana matumaini kuwa ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV jijini Barcelona nchini Hispania itakuwa chachu ya kufufua imani, matumaini na mshikamano wa waamini.
Akizungumza na Vatican News, Sister Anne amesema Hispania ni moja ya mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele kutuma wamisionari duniani kote kuhubiri Injili ya Kristo, na kwamba hata yeye alipata kumjua Mungu kupitia ushuhuda wa wamisionari hao.
Sister Anne, ambaye anafanya utume wake Barcelona kama mwalimu na mkufunzi wa Katekisimu, amesema sasa ni wakati wa kurudisha zawadi ya imani kwa kushiriki katika kazi ya uinjilishaji ndani ya Kanisa lililowahi kupeleka wamisionari barani Afrika.
Ameeleza kuwa Shirika la Watumishi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, lililoanzishwa mjini Vic, Barcelona mwaka 1891, limejikita katika elimu, maendeleo ya vijana na huduma kwa watu wenye mahitaji mbalimbali kwa kuiga mfano wa Kristo wa upendo na huruma.
Kuhusu ziara ya Papa Leo XIV, Sister Anne amesema anatamani iwe mwanzo wa upyaisho wa kiroho kwa Kanisa, huku akiwa na matumaini kwamba wale waliojitenga na Kanisa watagundua tena furaha ya kuwa sehemu ya jumuiya ya waamini.
Aidha amesema uwepo wa Baba Mtakatifu unaweza kuwahamasisha vijana kuitikia kwa ujasiri miito mbalimbali ya maisha ikiwemo ndoa, utawa na huduma kwa jamii.
Sister Anne amesisitiza kuwa ujumbe wa Papa Leo XIV unawakumbusha waamini kwamba wao ni sehemu ya familia moja ya Kanisa la ulimwengu, iliyounganishwa katika sala, utume na upendo wa Kristo, huku akiomba ziara hiyo iwe sauti ya kuhimiza haki, amani na mshikamano katika dunia ya leo.
