Na Shafiru Yusufu- Muleba, KAGERA
Halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera imeweza kukusanya jumla ya tani 5821 za Kahawa zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa msimu wa mwaka 2025/2026.
Mkaguzi wa zao la Kahawa wilaya ya Muleba Bw. Daudi Kingu amesema hayo kwenye kikao cha wadau wa Kahawa ambapo amesema kuwa halmashauri imeweza kukusanya ushuru wa shilingi milioni 817.

Amesema kuwa awali walikisia kukusanya tani 5,816 na kukusanya ushuru shilingi milioni 500 hivyo ongezeko hilo limetokana na bei ya kahawa sokoni pamoja na usimamizi mzuri wa makusanyo.
Bw. Kingu amesema kwa msimu wa mwaka huu wanalenga kukusanya jumla ya tani 6,598 za Kahawa zenye thamani shilingi bilioni 26 huku ushuru wa Halmashauri ukiwa shilingi milioni 791.
Akiongoza kikoa hicho Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga ameagiza kahawa zote ziuzwe kwenye vyama vya msingi kupitia kwenye minada pamoja na mashine zote za kukoboa zitakoboa kahawa zilizonunuliwa mnadani.
Nao baadhi ya wadau wa kahawa wameshauri kudhibiti changamoto ya kuvuna kahawa mbichi ambayo imekuwa ikipelekea kushuka kwa thamani ya zao hilo la kahawa ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara pamoja na kudhibiti magendo ya kahawa.
Hamashauri ya Wilaya ya Muleba ina jumla ya vitalu 11 vya kuzalisha miche bora ya kahawa ambapo kwa mwaka jana imeweza kugawa bure jumla ya miche 2,944,178 kwa wakulima.

