Rais wa Kenya, William Ruto, ametoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uhuru wa usafiri wa watu, bidhaa na huduma, akisisitiza kuwa mshikamano wa kikanda haupaswi kuzuiliwa na mipaka ya kisiasa.
Rais Ruto amesema hayo jijini Dodoma leo Mei 5, 2026, wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni hitimisho la ziara yake ya kikazi ya siku mbili nchini.
Katika hotuba yake, amesema wananchi wa Afrika Mashariki tayari wameunganishwa kupitia uhusiano wa kifamilia, biashara na shughuli za kiuchumi zinazovuka mipaka, hivyo sera za nchi zinapaswa kuendana na uhalisia huo.
Ameeleza kuwa katika ukanda huo wapo wananchi wengi wenye familia pande zote za mipaka, huku wafanyabiashara na wajasiriamali wakitegemea usafirishaji rahisi wa bidhaa na huduma ili kuendeleza shughuli zao.
Akitoa mfano wa umoja wa asili, Rais Ruto ametaja uhamaji wa wanyamapori kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na Maasai Mara, akisema mamilioni ya wanyama husafiri kila mwaka bila kujali mipaka ya nchi.
Aidha, ametoa rai kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujifunza kutokana na historia ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo mwaka 1977, akieleza kuwa changamoto zilizojitokeza zilikuwa za kiutendaji na zinaweza kuepukika.
Rais Ruto amesisitiza kuwa kuna haja ya dhamira ya dhati na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha Afrika Mashariki inakuwa na umoja imara unaowanufaisha wananchi wake wote.
