Na Enock Yoronimo- Bukoba, Kagera
Serikali kupitia wakala wa Nishati vijijini REA imesema ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia inatakiwa kuwahusisha wadau wa nishati safi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Mwandamizi wa REA, Deusdedith Malulu, wakati akifanya utambulisho wa mtoa huduma ya nishati safi katika Ofisi ya mkuu wa mkoa Kagera ambae ni Burn Manufacturing Company Limited, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa majiko banifu kwa wananchi wa mkoa wa Kagera.
Jumla ya majiko banifu 12,000 yanatarajiwa kusambazwa katika Mkoa wa Kagera, huku kila jiko likiuzwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 12,500 ili kuhakikisha linapatikana kwa urahisi kwa wananchi wengi.

Malulu amesema kuwa REA itaendelea kushirikiana na wadau ili kufanikisha kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Yahya Ramadhani Kido, amesema juhudi za REA za kurahisisha upatikanaji wa nishati safi zitendelea kuleta suluhisho la kudumu katika kumaliza changamoto ya matumizi ya nishati zisizo safi ambazo ni Kuni pamoja na mkaa.

