Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohammed, amesema watahiniwa wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) wanatarajiwa kufanya mtihani huo kesho, Septemba 9 na 10, 2026.
Profesa Mohammed ameyasema hayo leo, Septemba 8, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za NECTA jijini Dar es Salaam.
Amesema jumla ya watahiniwa 1,168,649 wamesajiliwa kufanya mtihani huo katika shule 20,019 nchini, ambapo wavulana ni 531,467, sawa na asilimia 45.48, huku wasichana wakiwa 637,182, sawa na asilimia 54.52.
Kwa mujibu wa Profesa Mohammed, idadi ya wasichana waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni kubwa kwa watahiniwa 105,715 ikilinganishwa na wavulana.
Amesema kati ya watahiniwa wote, 1,081,204, sawa na asilimia 92.52, watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, huku 87,445, sawa na asilimia 7.48, wakifanya kwa lugha ya Kiingereza.
Aidha, amesema watahiniwa wenye mahitaji maalumu ni 4,867, ambapo 82 ni wasioona, 1,551 wana uoni hafifu, 999 wana uziwi, 576 wana ulemavu wa akili na 1,659 wana ulemavu wa viungo.
Amesema watahiniwa watafanya mitihani katika masomo mbalimbali, ikiwemo Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili.
