Na Enock Yoronimo- Bukoba, KAGERA
Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini pamoja na wadau wa usafiri huo wameiomba serikali kusimamia na kurekebisha hali ya upandaji wa mafuta kihorera ili kupunguza uwezekano wa kupanda kwa nauli.
Wasema hayo katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wasafiri na wamiliki wa vyombo vya usafili majini pamoja viongozi wa serikali ambao umeratibiwa na Shirika la Wakala Meli Tanzania TASAC uliofanyika mjini Bukoba.

Wamesema kuwa hali inavyoonekana upo uwezekano wa kupanda kwa nauli wakisema hatua hiyo itaongeza ugumu wa maisha huku wakiiomba serikali kutafuta mwaarobaini wa kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
Wadau hao wamekutana kwa lengo la kujadili na kutathmini uwezekano wa kurekebisha au kuongeza nauli za abiria kufuatia kupanda kwa bei elekezi ya mafuta iliyoanza kutumika Aprili Mosi mwaka huu.
Afisa Uhusiano wa TASAC Kanda ya Ziwa, Said Mkabakuli, amesema kuwa ongezeko la bei ya mafuta limeathiri gharama za uendeshaji wa vyombo vya majini, hali inayolazimu kufanyika kwa tathmini bila kuathiri wadau.
Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Kagera, Isaya Tendega, ambae alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesisitiza kuwa mapendekezo ya wadau yamepokelewa na kufikishwa katika mamlaka husika na majibu kurejeshwa kwa wadau kabla ya Aprili 26, 2026 kwa ajili ya hatua zaidi za maamuzi.
