Msanii wa Hip Hop nchini, Chidi Benz, ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuurudia upya wimbo wake maarufu wa “Dar es Salaam Stand Up” aliouachia miaka ya nyuma msanii huyo amesema wazi kuwa haoni sababu ya kuufanyia remax wimbo huo kwa sasa.
Chidi Benz pia amekanusha kauli yake ya zamani iliyowahi kueleza uwezekano wa kushirikiana na Rayvanny katika kuurudia wimbo huo. Msanii huyo amesema kuwa huenda wakati huo hakumaanisha alichokisema, akieleza kwa utani kwamba “labda nililewa, siwezi kuirudia.”
Katika mahojiano hayo, Chidi Benz amezungumzia pia mafanikio yake kwenye tuzo za muziki wa Hip Hop Tanzania ambapo alifanikiwa kuondoka na tuzo tano. Msanii huyo amesema kuwa ushindani ulikuwa mkubwa sana na hakuna tuzo aliyopata kwa urahisi kutokana na kuwepo kwa wasanii wengi wakubwa waliokuwa wakishindana naye.
Aidha, Chidi Benz alisema ushindi wake umeonyesha uwezo wake mkubwa kwenye muziki wa Hip Hop, hasa kutokana na mara nyingi kulinganishwa na wasanii wengine wanaotajwa kuwa wakali zaidi yake. Alisisitiza kuwa kazi na mchango wake kwenye muziki vinaendelea kuthibitisha nafasi yake ndani ya tasnia hiyo.
Mbali na hayo, Chidi Benz ameweka wazi kuwa hayupo tayari kusainiwa na mtu yeyote au kampuni yoyote ya muziki licha ya uwepo wa tetesi zilizowahi kumhusisha na Chief Godlove. Msanii huyo amesema kuwa hakuna mtu mwenye uwezo wa kumsaini “hata awe na pesa kiasi gani,” akisisitiza kuwa anataka kubaki huru katika kufanya muziki wake.
