Kundi maarufu la watoto wanaocheza dansi kutoka Uganda, Ghetto Kids, limeendelea kuandika historia baada ya kupata nafasi ya kushiriki kwenye halftime show ya fainali ya Kombe la Dunia 2026 kupitia mwaliko maalum kutoka kwa msanii wa kimataifa Shakira.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Shakira aliwatangaza rasmi Ghetto Kids kuwa kundi la kwanza alilochagua kushirikiana nalo katika burudani ya fainali hiyo kubwa ya dunia itakayofanyika kwa pamoja nchini Marekani, Canada na Mexico.
Ghetto Kids ambao walitokea katika mitaa ya Katwe Slums jijini Kampala, wamepata umaarufu mkubwa duniani kutokana na vipaji vyao vya dansi na ubunifu wao wa kipekee, hali iliyowahi kuwafanya kushiriki pia katika mashindano ya America’s Got Talent.
Baadhi ya wanakundi hilo wameeleza furaha yao baada ya kupata nafasi hiyo wakisema ni hatua kubwa katika maisha yao na inaweza kuwafungulia milango zaidi kwenye tasnia ya burudani kimataifa.
Mashabiki wengi barani Afrika wameendelea kuwapongeza Ghetto Kids kwa mafanikio hayo huku wakieleza kuwa ni mfano wa kuigwa kwa vijana wenye vipaji wanaotoka kwenye mazingira magumu.
