Wananchi wa vijiji vya Mnazi, Milamba na Nalingu wilayani Mtwara wamepinga uwekezaji wa kilimo cha mwani unaotarajiwa kufanywa na mwekezaji kutoka China wakidai hawakushirikishwa ipasavyo kabla ya kuanza kwa shughuli za mradi huo.
Wakizungumza katika mkutano wa kijiji uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, wananchi hao walisema hawajapatiwa taarifa za kutosha kuhusu uwekezaji huo pamoja na athari zake kwa shughuli zao za uvuvi na maisha ya kila siku.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Nalingu, wameeleza kuwa hatua ya mwekezaji kuanza shughuli bila kushirikisha jamii imezua hofu na sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Wamedai eneo linalotarajiwa kutumika kwa kilimo hicho ni sehemu muhimu kwa shughuli za uvuvi ambazo ndizo chanzo kikuu cha kipato kwa wananchi wengi wa maeneo hayo.
Baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, aliamuru kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za uwekezaji huo hadi wananchi watakaposhirikishwa rasmi na kupewa maelezo ya kina kuhusu mradi huo.
