Papa Leo XIV amemteua Antonio Di Iorio kuwa Mkurugenzi mpya wa Mfuko wa Usaidizi wa Afya wa Vatican (FAS), taasisi inayotoa huduma za afya kwa wafanyakazi wa Kikanisa, watawa, walei pamoja na wastaafu wa Curia Romana na taasisi nyingine zinazosimamiwa na Kiti Kitakatifu cha Kitume.
Taarifa ya uteuzi huo ilichapishwa Mei 28, 2026 na kutangazwa katika Sekretarieti ya Vatican na Naibu wake, Paolo Rudelli, Kabla ya uteuzi huo, Di Iorio alikuwa akihudumu katika Kitengo cha Masuala ya Jumla cha Sekretarieti ya Vatican na ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya FAS tangu mwaka 2020, Anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake mapya Julai 15 mwaka huu.
Di Iorio, ambaye ameoa na ana mtoto mmoja wa kiume, ameihudumia Vatican kwa zaidi ya miaka 38 tangu alipoajiriwa Januari 2, 1988. Katika kipindi hicho ameshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na ukaguzi ndani ya taasisi za Vatican, huku pia akihudumu kama mthibitishaji wa saini katika Ofisi ya Camerlengo.
Aidha, ameshiriki mara mbili katika shughuli za uchaguzi wa Papa, kufuatia kujiuzulu kwa Benedict XVI na baada ya kifo cha Francis. Kutokana na mchango wake, Di Iorio ametunukiwa tuzo za kipapa za Mtakatifu Sylvester mwaka 1994 na Mtakatifu Gregori Mkuu mwaka 2006.
