Miaka 13 tangu kufariki kwa rapa wa Tanzania Albert Mangwea maarufu kama Ngwea, mashabiki wa muziki wanaendelea kumkumbuka kama mmoja wa wasanii waliobadilisha kabisa taswira ya Hip Hop Bongo.
Ngwea aliyefariki dunia Mei 28 mwaka 2013, alijulikana kwa uwezo mkubwa wa freestyle, mashairi yenye uhalisia wa maisha ya mtaani pamoja na style yake ya kipekee iliyomtofautisha na wasanii wengine wa kizazi chake.
Katika maisha yake ya muziki, Mangwea aliachia kazi nyingi zilizopata mafanikio makubwa ndani na nje ya Tanzania zikiwemo CNN, Mafia, Kimyakimya, Nipe Deal, Kimyakimya, Speed 120 pamoja na Tupo Juu.
Wasanii na mashabiki wengi wameendelea kueleza kuwa Ngwea alikuwa na kipaji cha kipekee na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa muziki wa Hip Hop nchini, huku baadhi wakimfananisha na rap legend wa Marekani 2Pac kutokana na ushawishi wake mkubwa kwenye muziki na jamii.
Mpaka leo, nyimbo na mchango wa Mangwea vinaendelea kuishi kwenye historia ya muziki wa Tanzania kama sehemu muhimu ya maendeleo ya Hip Hop Bongo.
