Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amezitaka halmashauri za mkoa huo kuandaa sheria ndogo zitakazodhibiti ununuzi holela wa mazao ili kuwalinda wakulima dhidi ya wanunuzi wanaojipangia bei.
Akizungumza katika mikutano ya mabaraza ya madiwani ya Halmashauri za Kibondo na Kakonko iliyojadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Sirro amesema baadhi ya wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakiwapangia wakulima bei zisizo na tija, hali inayowadidimiza kiuchumi.
Pia amezielekeza halmashauri kuhakikisha zinawalipa wazabuni kwa wakati, akisema ucheleweshaji wa malipo huchangia baadhi yao kufilisika na kushindwa kuendelea kutoa huduma.
Aidha, amezipongeza halmashauri za Kibondo na Kakonko kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
