Mdahalo kuhusu hatua ambazo Tanzania inazidi kupiga katika kufanikisha lengo la kuwafanya asilimia 80 ya wananchi wake wanatumia Nishati Safi katika shughuli za kila siku umeonesha kuwa taasisi zinazotekeleza mkakati huo zinafanikiwa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Jadidifu kutoka Wakala wa Nishati Vijiji (REA), Mhandisi, Advera Mwijage wakati wa mdahalo wa tathmini ya kasi ya usambazaji wa miundombinu na uwezeshaji wa matumizi ya nishati hiyo kwa wananchi wa kada mbalimbali uliofanyika katika Tamasha la Kizimkazi, mkoa wa Kusini Unguja, visiwani Zanzibar.
“REA imeendelea kuchukua hatua mbalimbali na tumefanikiwa kusambaza mitungi laki saba ya gesi ya kupikia (LPG) nchini kote, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kasi wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.” Amesema Mhandisi Advera kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.
Mhandisi Advera ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwezeshaji kutoka kwa Serikali ya Awamu ya Sita, sambamba na uwepo wa vyanzo vingi vya nishati nchini.
Katika hatua nyingine Mhandisi Advera amesema kuwa REA imeanzisha mradi wa kusambaza majiko banifu na kufungua viwanda vya kuzalisha mkaa mbadala maeneo ya vijijini kwa kushirikiana na STAMICO ili kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji holela wa misitu unaokadiriwa kufikia hekta 470,000 kwa mwaka kwa ajili ya kuni na mkaa.
Mdahalo huo umehudhuriaa na viongozi waandamizi wa sekta ya nishati, akiwemo Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Salome Makamba, na Katibu Mkuu (Umeme na Nishati Jadidifu) Mhandisi Felchesmi Mramba sambamba na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange.

katika picha ni Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi hii leo August 12,2026 Zanzibar
